Hesabu - Sura ya 30

Hesabu - Sura ya 30

1Kisha Musa akanena na wale vichwa vya kabila za wana wa Israeli, na kuwaambia, Neno hili ndilo aliloliagiza Bwana.

2Mtu atakapomwekea Bwana nadhiri, au, atakapoapa kiapo ili kufunga nafsi yake kwa kifungo, asilitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake.

3Tena mtu mke atakapomwekea Bwana nadhiri, na kufunga nafsi yake kwa kifungo, naye aketi katika nyumba ya babaye, katika ujana wake;

4babaye naye akasikia nadhiri yake, na kile kifungo chake alichofungia nafsi yake, na babaye akamnyamazia; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichofungia nafsi yake kitathibitika.

5Lakini kama huyo babaye akimkataza siku hiyo aliyosikia; nadhiri zake ziwazo zote, wala vifungo vyake alivyoifungia nafsi yake havitathibitika; na Bwana atamsamehe, kwa kuwa babaye alimkataza.

6Tena kama amekwisha kuolewa na mume, wakati huo wa nadhiri zake, au wa neno hilo alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia;

7na mumewe akasikia, naye akamnyamazia siku hiyo aliyosikia neno hilo; ndipo nadhiri zake zitathibitika, na vile vifungo ambavyo ameifunga nafsi yake vitathibitika.

8Lakini kama mumewe akimkataza siku hiyo aliyolisikia; ndipo ataitangua nadhiri yake iliyo juu yake na neno alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia; na Bwana atamsamehe

9Lakini nadhiri ya mjane, au ya mwanamke aliyeachishwa mume, kila neno ambalo ameifunga nafsi yake kwalo, litathibitika juu yake.

10Tena kama aliweka nadhiri nyumbani mwa mumewe, au kama aliifunga nafsi yake kwa kifungo pamoja na kiapo,

11na mumewe alisikia akamnyamazia, wala hakumkataza; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichojifungia kitathibitika.

12Lakini kama mumewe alizibatilisha na kuzitangua siku hiyo aliyozisikia, ndipo kila neno lililotoka midomoni mwake katika hizo nadhiri zake, au katika kile kifungo cha nafsi yake, halitathibitika; huyo mumewe amezitangua; na Bwana atamsamehe.

13Kila nadhiri, na kila kiapo kifungacho, ili kuitaabisha nafsi ya mwanamke mumewe aweza kuthibitisha, au mumewe aweza kutangua.

14Lakini mumewe akimnyamazia mkewe kabisa siku hata siku ndipo azithibitisha nadhiri zote za mkewe, au vifungo vyake vyote vilivyo juu yake; yeye amezithibitisha, kwa kuwa alimnyamazia mkewe siku hiyo aliyozisikia nadhiri zake.

15Lakini akizibatilisha na kuzitangua baada ya kuzisikia; ndipo yeye atachukua uovu wa mkewe.

16Hizi ndizo amri, ambazo Bwana alimwagiza Musa, kati ya mtu mume na mkewe, kati ya baba na binti yake, katika ujana wake, ali nyumbani mwa babaye.