Hesabu - Sura ya 5

1Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2Waamrishe wana wa Israeli kwamba wamtoe kila mwenye ukoma maragoni, na kila mtu aliye na kisonono, na kila aliye najisi kwa ajili ya wafu;
3mtawatoa nje wote, waume kwa wake, mtawaweka nje ya marago; ili wasiyatie unajisi marago yao, ambayo mimi naketi katikati yake.
4Wana wa Israeli wakafanya vivyo, wakawatoa na kuwaweka nje ya marago; kama Bwana alivyonena na Musa, ndivyo walivyofanya wana wa Israeli.
5Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
6Uwaambie wana wa Israeli, Mtu mume au mke atakapofanya dhambi yo yote, ifanywayo na binadamu, kumwasi Bwana, na mtu huyo akawa na hatia;
7ndipo watakapoungama dhambi yao waliyoifanya; naye atarudisha kwa hatia yake, kwa utimilifu wake, tena ataongeza juu yake sehemu ya tano, na kumpa huyo aliyemkosa.
8Lakini kwamba mtu huyo hana jamaa ya karibu ambaye inampasa kurudishiwa kwa ajili ya hiyo hatia, kile kitakachorudishwa kwa Bwana kwa hiyo hatia kitakuwa cha kuhani, pamoja na kondoo mume wa upatanisho, ambaye kwa huyo utafanywa upatanisho kwa ajili yake.
9Tena kila sadaka ya kuinuliwa, ya vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, watakavyosongeza kwa kuhani, itakuwa ni yake.
10Tena vitu vilivyowekwa wakfu na mtu awaye yote, vitakuwa ni vya kuhani; kitu cho chote mtu atakachompa kuhani, kitakuwa chake.
11Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
12Nena na wana wa israeli, uwaambie, kama mke wa mtu ye yote akikengeuka, na kumkosa mumewe,
13na mtu mume akalala naye kwa uasherati, na jambo hilo likamfichamania mumewe, likawa jambo lisilojulikana, na huyo mwanamke akawa najisi, wala hapana shahidi aliyeshuhudia juu yake, wala hakufumaniwa;
14kisha mumewe akashikwa na roho ya wivu, akamwonea wivu mkewe, naye akawa najisi huyo mwanamke; au kama akiingiwa na roho ya wivu, akamwonea wivu mkewe, naye hakuwa na unajisi huyo mke;
15ndipo huyo mume atamchukua mkewe, aende naye kwa kuhani, naye ataleta sadaka yake kwa ajili yake, yaani, sehemu ya kumi ya efa ya unga wa shayiri; asitie mafuta juu yake, wala asitie ubani juu yake; maana, ni sadaka ya unga ya wivu, ni sadaka ya unga ya ukumbusho ya kukumbukia uovu.
16Basi kuhani atamleta mwanamke akaribie, na kumweka mbele za Bwana;
17kisha kuhani atatwaa maji matakatifu katika chombo cha udongo; kisha kuhani atatwaa katika vumbi lililo pale chini ya maskani, na kulitia katika hayo maji;
18kisha kuhani atamweka mwanamke mbele za Bwana, naye atazifungua nywele za kichwani mwa huyo mwanamke, kisha atampa hiyo sadaka ya unga ya ukumbusho mikononi mwake, ambayo ni sadaka ya unga ya wivu, naye kuhani atakuwa na hayo maji ya uchungu yaletayo laana mkononi mwake;
19tena kuhani atamwapisha huyo mwanamke, naye atamwambia mwanamke, Kwamba hakulala mtu mume pamoja nawe, tena kwamba hukukengeuka kuandama uchafu, uli chini ya mumeo, maji haya ya uchungu yaletayo laana yasikudhuru;
20lakini kwamba umekengeuka uli chini ya mumeo, na kwamba u hali ya unajisi, na mtu mume amelala nawe, asiyekuwa mumeo;
21hapo ndipo kuhani atamwapisha mwanamke kwa kiapo cha kuapiza, kisha kuhani atamwambia huyo mwanamke maneno haya, Bwana na akufanye wewe uwe laana na kiapo kati ya watu wako, hapo Bwana akufanyapo paja lako kupooza, na tumbo lako kuvimba;
22na maji yaletayo laana yatakuingia matumboni mwako, na kukuvimbisha tumbo, na kukupoozesha paja lako; na mwanamke ataitika, Amina, Amina.
23Kisha kuhani ataziandika laana hizo ndani ya kitabu, na kuzifuta katika maji ya uchungu;
24kisha atamnywesha mwanamke hayo maji ya uchungu yaletayo laana; nayo maji yaletayo laana yataingia ndani yake, nayo yatageuka kuwa uchungu.
25Kisha kuhani ataitwaa hiyo sadaka ya unga ya wivu, kwa kuiondoa mkononi mwa huyo mwanamke, naye ataitikisa sadaka ya unga mbele ya Bwana, na kuisongeza pale madhabahuni;
26kisha kuhani atatwaa konzi moja ya sadaka ya unga, kuwa ni ukumbusho wake, na kuuteketeza madhabahuni, baadaye atamnywesha mwanamke hayo maji.
27Kisha hapo atakapokwisha kumnywesha maji, ndipo itakapokuwa, kama amekuwa hali ya unajisi na kumkosa mumewe, hayo maji yaletayo laana yatamwingia ndani yake, nayo yatakuwa uchungu, na tumbo lake litavimba, na paja lake litapooza; na huyo mwanamke atakuwa laana kati ya watu wake.
28Na kama mwanamke hakuwa na unajisi lakini yu safi; ndipo ataachiliwa, naye atazaa wana.
29Hii ndiyo sheria ya wivu, mwanamke, ambaye yu chini ya mumewe, akikengeuka, na kupata unajisi;
30au, roho ya wivu ikimwingia mtu mume, naye akamwonea wivu mkewe; ndipo atakapomweka huyo mwanamke mbele za Bwana, na kuhani atatenda juu yake sheria hii yote.
31Na huyo mume atakuwa hana uovu, na mwanamke atauchukua uovu wake.