Mithali - Sura ya 10

1Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye.
2Hazina za uovu hazifaidii kitu; Bali haki huokoa na mauti.
3Bwana hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa; Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali.
4Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.
5Akusanyaye wakati wa hari ni mwana mwenye hekima; Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.
6Baraka humkalia mwenye haki kichwani; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu.
7Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka; Bali jina la mtu mwovu litaoza.
8Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.
9Aendaye kwa unyofu huenda salama; Bali apotoshaye njia zake atajulikana.
10Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.
11Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu,
12Kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote.
13Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu; Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu.
14Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.
15Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Uangamivu wa maskini ni umaskini wao.
16Kazi yake mwenye haki huuelekea uzima; Mazao ya wabaya huuelekea dhambi.
17Akubaliye kurudiwa huwa katika njia ya uzima; Bali yeye aachaye maonyo hukosa.
18Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.
19Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.
20Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha teule; Moyo wa mtu mbaya haufai kitu.
21Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi; Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu.
22Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.
23Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo; Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima.
24Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia; Na wenye haki watapewa matakwa yao.
25Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena; Bali mwenye haki ni msingi wa milele.
26Kama siki menoni, na kama moshi machoni, Ndivyo alivyo mtu mvivu kwao wamtumao.
27Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.
28Matumaini yao wenye haki yatakuwa furaha; Bali kutaraji kwao wasio haki kutapotea.
29Njia ya Bwana ni kimbilio lake mtu mkamilifu; Bali ni uharibifu kwao watendao maovu.
30Mwenye haki hataondolewa milele; Bali wasio haki hawatakaa katika nchi.
31Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima; Bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali.
32Midomo ya mwenye haki huyajua yatakayokubaliwa; Bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi.