Mithali - Sura ya 12

Mithali - Sura ya 12

1Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa; Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama.

2Mtu mwema atapata upendeleo kwa Bwana; Bali mtu wa hila atahukumiwa naye.

3Mtu hatathibitika kwa njia ya uovu; Shina la mwenye haki halitaondolewa kamwe.

4Mwanamke mwema ni taji ya mumewe; Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake.

5Mawazo ya mwenye haki ni adili; Bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa.

6Maneno ya waovu huotea damu; Bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa.

7Waovu huangamia, hata hawako tena; Bali nyumba ya mwenye haki itasimama.

8Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake; Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa.

9Afadhali mtu anayedharauliwa, ikiwa ana mtumwa, Kuliko ajisifuye, ikiwa anahitaji chakula.

10Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.

11Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi hana ufahamu.

12Asiye haki hutamani nyavu za wabaya; Bali shina lao wenye haki huleta matunda.

13Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya; Bali mwenye haki atatoka katika taabu.

14Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake; Na atarudishiwa matendo ya mikono yake.

15Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.

16Ghadhabu ya mpumbavu hujulika mara; Bali mtu mwerevu husitiri aibu.

17Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila.

18Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; Bali ulimi wa mwenye haki ni afya.

19Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.

20Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu; Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.

21Mwenye haki hatapatikana na msiba wo wote; Bali wasio haki watajazwa mabaya.

22Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake.

23Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa; Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu.

24Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi.

25Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha; Bali neno jema huufurahisha.

26Mwenye haki ni kiongozi cha mwenzake; Bali njia ya wasio haki huwakosesha.

27Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anazo mali za thamani.

28Katika njia ya haki kuna uhai; Wala hakuna mauti katika mapito yake.