Mithali - Sura ya 13

Mithali - Sura ya 13

1Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.

2Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri.

3Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu.

4Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa.

5Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu.

6Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake; Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi.

7Kuna mtu mwenye kujitajirisha, lakini hana kitu; Kuna ajifanyaye kuwa maskini, lakini ana mali nyingi.

8Dia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake; Bali mtu maskini hasikii ogofyo lo lote.

9Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika.

10Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.

11Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa.

12Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.

13Kila alidharauye neno hujiletea uharibifu; Bali yeye aiogopaye amri atapewa thawabu.

14Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti.

15Ufahamu mwema huleta upendeleo; Bali njia ya haini huparuza.

16Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali mpumbavu hueneza upumbavu.

17Mjumbe mbaya huanguka maovuni; Bali mjumbe mwaminifu ni afya.

18Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa; Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa.

19Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu; Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu.

20Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.

21Uovu huwaandamia wenye dhambi; Bali mwenye haki atalipwa mema.

22Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki.

23Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini; Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma.

24Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; Bali yeye ampendaye humrudi mapema.

25Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake; Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa.