Mithali - Sura ya 14

Mithali - Sura ya 14

1Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.

2Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha Bwana; Bali aliye mkaidi katika njia zake humdharau.

3Katika kinywa cha mpumbavu mna fimbo ya kiburi, Bali midomo ya wenye hekima huwahifadhi.

4Zizi ni safi ambapo hapana ng'ombe; Bali nguvu za ng'ombe zaleta faida nyingi.

5Shahidi mwaminifu hatasema uongo; Bali shahidi wa uongo, pumzi zake ni uongo.

6Mwenye dharau hutafuta hekima, asiipate; Bali maarifa huwa mepesi kwa mwenye ufahamu.

7Toka mbele ya uso wa mpumbavu, Maana hutaona kwake midomo ya maarifa.

8Akili za mwenye busara ni kujua njia yake; Lakini upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.

9Wapumbavu huidharau hatia; Bali upo upendeleo kwa wenye haki.

10Moyo huujua uchungu wa nafsi yake, Wala mgeni haishiriki furaha yake.

11Nyumba ya mtu mbaya itabomolewa; Bali hema ya mwenye haki itafanikiwa.

12Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.

13Hata wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni; Na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo.

14Ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe; Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake.

15Mjinga huamini kila neno; Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.

16Mwenye hekima huogopa, akajitenga na uovu; Bali mpumbavu ana ufidhuli, na kujitumai.

17Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga; Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa.

18Wajinga hurithi upumbavu; Bali wenye busara huvikwa taji ya maarifa.

19Wabaya huinama mbele ya wema, Na wasio haki malangoni mwao wenye haki.

20Maskini huchukiwa hata na jirani yake; Bali tajiri ana rafiki wengi.

21Amdharauye mwenzake afanya dhambi; Bali amhurumiaye maskini ana heri.

22Je! Hawakosi wawazao mabaya? Bali fadhili na kweli zina wao wawazao mema.

23Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.

24Taji ya wenye hekima ni mali zao; Bali upumbavu wa wajinga ni upumbavu tu.

25Shahidi wa kweli huponya nafsi za watu; Bali atoaye uongo hudanganya.

26Kumcha Bwana ni tumaini imara; Watoto wake watakuwa na kimbilio.

27Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti.

28Utukufu wa mfalme ni wingi wa watu wake; Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao.

29Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi; Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu.

30Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili; Bali husuda ni ubovu wa mifupa.

31Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake; Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu.

32Mtu mbaya husukumwa chini katika kutenda mabaya kwake; Bali mwenye haki ana matumaini katika kufa kwake.

33Hekima hukaa katika moyo wake mwenye ufahamu; Bali yaliyo ndani ya wapumbavu hudhihirika.

34Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.

35Upendeleo wa mfalme humwelekea mtumwa atendaye kwa busara; Bali ghadhabu yake itakuwa juu yake aletaye aibu.