Mithali - Sura ya 15

Mithali - Sura ya 15

1Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.

2Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri; Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu.

3Macho ya Bwana yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema.

4Ulimi safi ni mti wa uzima; Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.

5Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye; Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara.

6Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi; Bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu.

7Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa; Bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo.

8Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.

9Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali humpenda mtu afuatiaye wema.

10Adhabu kali ina yeye aiachaye njia; Naye achukiaye kukemewa atakufa.

11Kuzimu na Uharibifu vi wazi mbele za Bwana; Si zaidi basi, mioyo ya wanadamu?

12Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa; Wala yeye hawaendei wenye hekima.

13Moyo wa furaha huchangamsha uso; Bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.

14Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa; Bali kinywa cha wapumbavu hula upumbavu.

15Siku zote za mtu ateswaye ni mbaya; Bali ukunjufu wa moyo ni karamu ya daima.

16Kuwa na mali chache pamoja na kumcha Bwana; Ni bora kuliko mali nyingi pamoja na taabu.

17Chakula cha mboga penye mapendano; Ni bora kuliko ng'ombe aliyenona pamoja na kuchukiana.

18Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.

19Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba; Bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu.

20Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mpumbavu humdharau mamaye.

21Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili; Bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake.

22Pasipo mashauri makusudi hubatilika; Bali kwa wingi wa washauri huthibithika.

23Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake; Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!

24Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu chini.

25Bwana ataing'oa nyumba ya mwenye kiburi; Bali atauthibitisha mpaka wa mjane.

26Mashauri mabaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maneno yapendezayo ni safi.

27Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe; Bali achukiaye zawadi ataishi.

28Moyo wa mwenye haki hufikiri jinsi atakavyojibu; Bali kinywa cha wasio haki humwaga mabaya.

29Bwana yu mbali na wasio haki; Bali huisikia sala ya mwenye haki.

30Mng'ao wa macho huufurahisha moyo; Habari njema huinenepesha mifupa.

31Sikio lisikilizalo lawama yenye uhai Litakaa kati yao wenye hekima.

32Akataaye maonyo huidharau nafsi yake mwenyewe; Bali yeye asikilizaye lawama hujipatia ufahamu.

33Kumcha Bwana ni maonyo ya hekima; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.