Mithali - Sura ya 19

Mithali - Sura ya 19

1Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa midomo aliye mpumbavu.

2Tena si vizuri nafsi ya mtu ikose maarifa; Naye afanyaye haraka kwa miguu hutenda dhambi.

3Upumbavu wa mtu hupotosha njia yake; Na moyo wake hununa juu ya Bwana.

4Utajiri huongeza rafiki wengi; Bali maskini hutengwa na rafiki yake.

5Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Wala asemaye uongo hataokoka.

6Watu wengi watamsihi mkuu ili awafadhili; Na kila mtu ni rafiki yake atoaye tunu.

7Ndugu zote wa maskini humchukia; Jinsi gani rafiki zake huzidi kujitenga naye! Huwafuata kwa maneno, lakini wametoweka.

8Apataye hekima hujipenda nafsi yake; Ashikaye ufahamu atapata mema.

9Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Naye asemaye uongo ataangamia.

10Maisha ya anasa hayampasi mpumbavu; Sembuse mtumwa awatawale wakuu.

11Busara ya mtu huiahirisha hasira yake; Nayo ni fahari yake kusamehe makosa.

12Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba; Bali hisani yake kama umande juu ya majani.

13Mwana mpumbavu ni msiba kwa babaye; Na ugomvi wa mke kama kutona-tona daima.

14Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.

15Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa.

16Yeye aihifadhiye amri huihifadhi nafsi yake; Bali yeye asiyeziangalia njia zake atakufa.

17Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana; Naye atamlipa kwa tendo lake jema.

18Mrudi mwanao, kwa maana liko tumaini; Wala usiikaze nafsi yako kwa kuangamia kwake.

19Mtu wa hasira nyingi atachukua adhabu yake, Maana ujapomwokoa huna budi kufanya tena.

20Sikiliza mashauri, ukapokee mafundisho, Upate kuwa na hekima siku zako za mwisho.

21Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.

22Haja ya mwanadamu ni hisani yake; Ni afadhali maskini kuliko mwongo.

23Kumcha Bwana huelekea uhai; Atakaa ameshiba; hatajiliwa na ubaya.

24Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini; Ila hataki hata kuupeleka kinywani pake.

25Mpige mwenye mzaha, na mjinga atapata busara; Mwonye mwenye ufahamu, naye atatambua maarifa.

26Apotezaye mali za babaye na kumfukuza mamaye, Ni mwana aaibishaye, na kuleta lawama.

27Mwanangu, acha kusikia mafundisho, Ukitaka tu kuyaasi maneno ya maarifa.

28Shahidi asiyefaa kitu hudhihaki hukumu, Na vinywa vya wasio haki humeza uovu.

29Hukumu zimewekwa tayari kwa wenye mzaha; Na mapigo kwa mgongo wa wapumbavu.