Mithali - Sura ya 2

Mithali - Sura ya 2

1Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu, Na kuyaweka akiba maagizo yangu;

2Hata ukatega sikio lako kusikia hekima, Ukauelekeza moyo wako upate kufahamu;

3Naam, ukiita busara, Na kupaza sauti yako upate ufahamu;

4Ukiutafuta kama fedha, Na kuutafutia kama hazina iliyositirika;

5Ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, Na kupata kumjua Mungu.

6Kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu;

7Huwawekea wanyofu akiba ya hekima kamili; Yeye ni ngao kwao waendao kwa ukamilifu;

8Apate kuyalinda mapito ya hukumu, Na kuhifadhi njia ya watakatifu wake.

9Ndipo utakapofahamu haki na hukumu, Na adili, na kila njia njema.

10Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;

11Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi.

12Ili kukuokoa na njia ya uovu, Na watu wanenao yaliyopotoka;

13Watu waziachao njia za unyofu, Ili kuziendea njia za giza;

14Wafurahio kutenda mabaya; Wapendezwao na upotoe wa waovu;

15Waliopotoka katika njia zao; Walio wakaidi katika mapito yao.

16Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake;

17Amwachaye rafiki wa ujana wake, Na kulisahau agano la Mungu wake.

18Maana nyumba yake inaelekea mauti, Na mapito yake yanakwenda kwenye wafu.

19Katika hao wamwendeao harudi hata mmoja, Wala hawazifikilii njia za uzima.

20Ili upate kwenda katika njia ya watu wema, Na kuyashika mapito ya wenye haki.

21Maana wanyofu watakaa katika nchi, Na wakamilifu watadumu ndani yake.

22Bali waovu watatengwa na nchi, Nao wafanyao hila watang'olewa.