Mithali - Sura ya 21

Mithali - Sura ya 21

1Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo.

2Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huipima mioyo.

3Kutenda haki na hukumu Humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka.

4Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, Hata ukulima wa waovu, ni dhambi.

5Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji.

6Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti.

7Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali; Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu.

8Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana; Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa.

9Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.

10Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu; Jirani yake hapati fadhili machoni pake.

11Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa.

12Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia.

13Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa.

14Kipawa cha siri hutuliza hasira; Na rushwa bindoni humliza ghadhabu kali.

15Ni furaha yao wenye haki kutenda hukumu; Lakini ni uharibifu kwao watendao maovu.

16Mtu aikosaye njia ya busara Atakaa katika mkutano wao waliokufa.

17Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri.

18Mtu asiye haki ni fidia ya wenye haki; Naye afanyaye hila ni badala ya watu wa adili.

19Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi.

20Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima; Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza.

21Aandamaye haki na fadhili, Ataona uhai na haki na heshima.

22Mwenye hekima huupandia mji wao wenye nguvu; Na kuziangusha nguvu za tumaini lao.

23Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu.

24Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi; Hutenda mambo katika majivuno ya kiburi chake.

25Matakwa yake mtu mvivu humfisha, Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi.

26Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa; Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi.

27Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya!

28Shahidi wa uongo atapotea; Bali mtu asikiaye atasema maneno yadumuyo.

29Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu; Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake.

30Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri, juu ya Bwana.

31Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; Lakini Bwana ndiye aletaye wokovu.