Mithali - Sura ya 28

Mithali - Sura ya 28

1Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.

2Kwa sababu ya maasi ya nchi wakuu wake huwa wengi; Bali kwa wenye ufahamu na maarifa hali ya nchi hudumishwa

3Mtu mhitaji awaoneaye maskini, Ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza chakula.

4Wao waiachao sheria huwasifu waovu; Bali wao waishikao hushindana nao.

5Watu wabaya hawaelewi na hukumu; Bali wamtafutao Bwana huelewa na yote.

6Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa njia angawa ni tajiri.

7Yeye aishikaye sheria ni mwana mwenye hekima; Bali aliye rafiki wa walafi humwaibisha babaye.

8Yeye azidishaye mali yake kwa riba na faida, Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini.

9Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, Hata sala yake ni chukizo.

10Kila mtu awapotezaye wenye haki katika njia mbaya, Ataanguka katika rima lake mwenyewe; Bali wakamilifu watarithi mema.

11Mtu tajiri ana hekima machoni pake mwenyewe; Bali maskini mwenye ufahamu humchunguza sana.

12Wenye haki washindapo, uko utukufu mwingi; Bali waovu waondokapo, watu hujificha.

13Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.

14Mwanadamu mwenye kicho yu heri sikuzote; Bali mshupavu wa moyo ataangukia madhara.

15Kama simba angurumaye, na dubu mwenye njaa; Ndivyo alivyo mtu mbaya awatawalaye maskini.

16Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana; Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake.

17Aliyelemewa na damu ya mtu Atalikimbilia shimo; wala mtu asimzuie.

18Aendaye kwa unyofu ataokolewa; Bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara.

19Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi atapata umaskini wa kumtosha.

20Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa.

21Kupendelea watu si kwema; Wala mtu kuasi kwa ajili ya kipande cha mkate.

22Mwenye husuda afanya haraka kuwa tajiri; Wala haufikiri uhitaji utakaomjilia.

23Amkemeaye mwenzake hatimaye atapata kibali; Zaidi ya mtu ajipendekezaye kwa ulimi wake.

24Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa; Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu.

25Mwenye nafsi ya kutamani huchochea fitina; Bali amtumainiye Bwana atawandishwa.

26Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga; Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa.

27Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu; Bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi.

28Wasio haki wainukapo, wanadamu hujificha; Bali waangamiapo, wenye haki huongezeka.