Mithali - Sura ya 29

1Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.
2Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; Bali mwovu atawalapo, watu huugua.
3Apendaye hekima humfurahisha babaye; Bali ashikamanaye na makahaba hutapanya mali.
4Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.
5Mwenye kujipendekeza kwa jirani yake, Hutandika wavu ili kuitega miguu yake.
6Kuna mtego katika kosa la mtu mbaya; Bali mwenye haki huimba na kufurahi.
7Mwenye haki huyaangalia madai ya maskini; Bali mtu mbaya hana ufahamu hata ayajue.
8Watu wenye dharau huwasha mji moto; Bali wenye hekima hugeuzia mbali ghadhabu.
9Mwenye hekima akijadiliana na mpumbavu; Akikasirika au akicheka, pia hapana raha.
10Wamwagao damu humchukia mtu mkamilifu; Bali wenye haki humtunza nafsi yake.
11Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote; Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.
12Mwenye kutawala akisikiliza uongo; Basi watumishi wake wote watakuwa waovu.
13Maskini na mdhalimu hukutana pamoja; Bwana huwatia nuru macho yao wote wawili.
14Mfalme awahukumuye maskini kwa uaminifu; Kiti chake cha enzi kitathibitika milele.
15Fimbo na maonyo hutia hekima; Bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye.
16Waovu wakiongezeka, maasi huongezeka; Bali wenye haki watayatazama maanguko yao.
17Mrudi mwanao naye atakustarehesha; Naam, atakufurahisha nafsi yako.
18Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.
19Haitoshi mtumwa kuonywa kwa maneno; Maana ajapoyafahamu hataitika.
20Je! Umemwona mtu mwenye kuhamaki katika maneno? Afadhali kumtumaini mpumbavu kuliko yeye.
21Amtunduiaye mtumwa wake tangu utoto, Mwisho wake atakuwa ni mwanawe.
22Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Na mtu mwenye ghadhabu huasi sana.
23Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa.
24Mshiriki wa mwivi huichukia nafsi yake mwenyewe; Asikia maapizo, wala hana neno.
25Kuwaogopa wanadamu huleta mtego; Bali amtumainiye Bwana atakuwa salama.
26Watu wengi hutafuta upendeleo wa mkuu; Bali hukumu ya kila mtu hutoka kwa Bwana
27Mtu aliye dhalimu ni chukizo kwa wenye haki; Na mnyofu wa mwenendo ni chukizo kwa waovu.