Mithali - Sura ya 3

1Mwanangu, usiisahau sheria yangu, Bali moyo wako uzishike amri zangu.
2Maana zitakuongezea wingi wa siku. Na miaka ya uzima, na amani.
3Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.
4Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu.
5Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.
7Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.
8Itakuwa afya mwilini pako,
9Mheshimu Bwana kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.
10Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.
11Mwanangu, usidharau kuadhibiwa na Bwana, Wala usione ni taabu kurudiwa naye.
12Kwa kuwa Bwana ampendaye humrudi, Kama vile baba mwanawe ampendezaye.
13Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu.
14Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi.
15Yeye ana thamani kuliko marijani, Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye.
16Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto.
17Njia zake ni njia za kupendeza sana, Na mapito yake yote ni amani.
18Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; Ana heri kila mtu ashikamanaye naye.
19Kwa hekima Bwana aliiweka misingi ya nchi; Kwa akili zake akazifanya mbingu imara;
20Kwa maarifa yake vilindi viligawanyika; Na mawingu yadondoza umande.
21Mwanangu, yasiondoke haya machoni pako, Shika hekima kamili na busara.
22Basi yatakuwa uzima kwa nafsi yako, Na neema shingoni mwako.
23Ndipo utakapokwenda katika njia yako salama, Wala mguu wako hautakwaa.
24Ulalapo hutaona hofu; Naam, utalala na usingizi wako utakuwa mtamu.
25Usiogope hofu ya ghafula, Wala uharibifu wa waovu utakapofika.
26Kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako, Naye atakulinda mguu wako usinaswe.
27Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, Ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda.
28Usimwambie jirani yako, Nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa; Nawe unacho kitu kile karibu nawe.
29Usiwaze mabaya juu ya jirani yako, Ambaye anakaa karibu nawe na kujiona salama.
30Usishindane na mtu bila sababu, Ikiwa hakukudhuru kwa lo lote.
31Usimhusudu mtu mwenye jeuri, Wala usiichague mojawapo ya njia zake.
32Maana mtu mkaidi ni chukizo kwa Bwana, Bali siri yake ni pamoja na wanyofu.
33Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki.
34Hakika yake huwadharau wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema.
35Wenye hekima wataurithi utukufu, Bali kukuzwa kwa wapumbavu ni fedheha.