Mithali - Sura ya 30

Mithali - Sura ya 30

1Maneno ya Aguri bin Yake; mausia mtu huyu aliyomwambia Ithieli, naam, Ithieli na Ukali.

2Hakika nimekuwa kama mnyama, wala si mtu; Wala sina ufahamu wa mwanadamu;

3Wala sikujifunza hekima; Wala sina maarifa ya kumjua Mtakatifu.

4Ni nani aliyepanda mbinguni na kushuka chini? Ni nani aliyekamata upepo kwa makonzi yake? Ni nani aliyeyafunga maji ndani ya nguo yake? Ni nani aliyefanya imara ncha zote za nchi? Jina lake ni nani? Na ni nani jina la mwanawe, kama wajua?

5Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio.

6Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.

7Mambo haya mawili nimekuomba; Usininyime [matatu] kabla sijafa.

8Uniondolee ubatili na uongo; Usinipe umaskini wala utajiri; Unilishe chakula kilicho kadiri yangu.

9Nisije nikashiba nikakukana, Nikasema, Bwana ni nani? Wala nisiwe maskini sana nikaiba, Na kulitaja bure jina la Mungu wangu.

10Usimchongee mtumwa kwa bwana wake; Asije akakulaani, ukaonekana una hatia.

11Kuna kizazi cha watu wamlaanio baba yao; Wala hawambariki mama yao.

12Kuna kizazi cha watu walio safi machoni pao wenyewe; Ambao hawakuoshwa uchafu wao.

13Kuna kizazi cha watu ambao macho yao yameinuka kama nini! Na kope zao zimeinuka sana.

14Kuna kizazi cha watu ambao meno yao ni panga; Na vigego vyao ni kama visu. Ili kuwala maskini waondolewe katika nchi, Na wahitaji katika wanadamu.

15Mruba anao binti wawili, Waliao, Nipe! Nipe! Kuna vitu vitatu visivyoshiba kamwe, Naam, vinne visivyosema, Basi!

16Kuzimu; na tumbo lisilozaa; Nchi isiyoshiba maji; na moto usiosema, Basi!

17Jicho la mtu amdhihakiye babaye, Na kudharau kumtii mamaye; Kunguru wa bondeni wataling'oa, Na vifaranga vya tai watalila.

18Kuna mambo matatu yaliyo ya ajabu kwangu, Naam, kuna manne nisiyoyafahamu.

19Mwendo wa tai katika hewa; Na mwendo wa nyoka juu ya mwamba; Mwendo wa merikebu katikati ya bahari; Na mwendo wa mtu pamoja na msichana.

20Hivyo ndivyo mwendo wa mwanamke mzinifu; Hula, akapangusa kinywa chake, Akasema, Sikufanya uovu.

21Kwa ajili ya mambo matatu nchi hutetemeka, Naam, kwa ajili ya manne haiwezi kuvumilia.

22Mtumwa apatapo kuwa mfalme; Mpumbavu ashibapo chakula;

23Mwanamke mwenye kuchukiza aolewapo; Na mjakazi aliye mrithi wa bibi yake.

24Kuna viumbe vinne duniani vilivyo vidogo; Lakini vina akili nyingi sana.

25Chungu ni watu wasio na nguvu; Lakini hujiwekea chakula wakati wa hari.

26Wibari ni watu dhaifu; Lakini hujifanyia nyumba katika miamba.

27Nzige hawana mfalme; Lakini huenda wote pamoja vikosi vikosi.

28Mjusi hushika kwa mikono yake; Lakini yumo majumbani mwa wafalme.

29Kuna watatu wenye mwendo wa kupendeza, Naam, wanne walio na mwendo mzuri.

30Simba aliye hodari kupita wanyama wote; Wala hajiepushi na aliye yote;

31Jimbi aendaye tambo; na beberu; Na mfalme ambaye haasiki.

32Ikiwa umefanya kipumbavu kwa kujikuza; Au ikiwa umewaza mabaya; Basi weka mkono wako juu ya kinywa chako.

33Kwa maana kupiga maziwa huleta siagi; Na kupiga pua hutokeza damu; kadhalika kuchochea hasira hutokeza ugomvi.