Mithali - Sura ya 31

Mithali - Sura ya 31

1Maneno ya mfalme Lemueli; mausia aliyofundishwa na mama yake.

2Ni nini, mwanangu? Tena ni nini, mwana wa tumbo langu? Tena, ni nini mwana wa nadhiri zangu?

3Usiwape wanawake nguvu zako; Wala moyo wako usiwape wale wawaharibuo wafalme.

4Ee Lemueli, kunywa mvinyo hakuwafai wafalme, hakuwafai wafalme; Wala haifai wakuu waseme, Ki wapi kileo?

5Wasije wakanywa na kuisahau sheria, Na kuipotosha hukumu ya mtu aliye taabuni.

6Mpe kileo yeye aliye karibu na kupotea; Kampe divai yeye aliye na uchungu nafsini.

7Anywe akausahau umaskini wake; Asiikumbuke tena taabu yake.

8Fumbua kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao;

9Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; Uwapatie maskini na wahitaji haki yao.

10Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani.

11Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.

12Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake.

13Hutafuta sufu na kitani; Hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo.

14Afanana na merikebu za biashara; Huleta chakula chake kutoka mbali.

15Tena huamka, kabla haujaisha usiku; Huwapa watu wa nyumbani mwake chakula; Na wajakazi wake sehemu zao.

16Huangalia shamba, akalinunua; Kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu.

17Hujifunga nguvu viunoni kama mshipi; Hutia mikono yake nguvu.

18Huona kama bidhaa yake ina faida; Taa yake haizimiki usiku.

19Hutia mikono yake katika kusokota; Na mikono yake huishika pia.

20Huwakunjulia maskini mikono yake; Naam, huwanyoshea wahitaji mikono yake.

21Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake; Maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu.

22Hujifanyia mazulia ya urembo; Mavazi yake ni kitani safi na urujuani.

23Mume wake hujulikana malangoni; Aketipo pamoja na wazee wa nchi.

24Hufanya nguo za kitani na kuziuza; Huwapa wafanya biashara mishipi.

25Nguvu na hadhi ndiyo mavazi yake; Anaucheka wakati ujao.

26Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake.

27Huangalia sana njia za watu wa nyumbani mwake; Wala hali chakula cha uvivu.

28Wanawe huondoka na kumwita heri; Mumewe naye humsifu, na kusema,

29Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote.

30Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa.

31Mpe mapato ya mikono yake, Na matendo yake yamsifu malangoni.