Mithali - Sura ya 4

Mithali - Sura ya 4

1Wanangu, yasikilizeni mausia ya baba yenu, Tegeni masikio mpate kujua ufahamu.

2Kwa kuwa nawapa mafundisho mazuri; Msiiache sheria yangu.

3Maana nalikuwa mwana kwa baba yangu, Mpole, mpenzi wa pekee wa mama yangu.

4Naye akanifundisha, akaniambia, Moyo wako uyahifadhi maneno yangu; Shika amri zangu ukaishi.

5Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu.

6Usimwache, naye atakuhifadhi; Umpende, naye atakulinda.

7Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu.

8Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia.

9Atakupa neema kuwa kilemba kichwani; Na kukukirimia taji ya uzuri.

10Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi.

11Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu.

12Uendapo, hatua zako hazitadhiikika, Wala ukipiga mbio hutajikwaa.

13Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako.

14Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya.

15Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako.

16Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu.

17Maana wao hula mkate wa uovu, Nao hunywa divai ya jeuri.

18Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing'aayo, Ikizidi kung'aa hata mchana mkamilifu.

19Njia ya waovu ni kama giza; Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho.

20Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu.

21Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako.

22Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote.

23Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.

24Kinywa cha ukaidi ukitenge nawe, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe.

25Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa.

26Ulisawazishe pito la mguu wako, Na njia zako zote zithibitike;

27Usigeuke kwa kuume wala kwa kushoto; Ondoa mguu wako maovuni.