Mithali - Sura ya 6

Mithali - Sura ya 6

1Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa rafiki yako, Ikiwa wewe na mgeni mmepana mikono,

2Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,

3Sasa, mwanangu, fanya hivi ukajiokoe, Kwa kuwa umejitia mkononi mwa jirani yako; Nenda ukanyenyekee, na kumsihi jirani yako.

4Usiache macho yako kupata usingizi, Wala kope za macho yako kusinzia.

5Ujiponye kama paa na mkono wa mwindaji, Na kama ndege katika mkono wa mtega mitego.

6Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima.

7Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu,

8Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.

9Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako?

10Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi!

11Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.

12Mtu asiyefaa kitu, mtu wa uovu; Huenda njiani mwenye kinywa cha upotofu.

13Hukonyeza kwa macho, hunena kwa miguu, Huwaashiria watu kwa vidole vyake.

14Mna upotofu moyoni mwake, hutunga uovu daima, Hupanda mbegu za magomvi.

15Basi msiba utampata kwa ghafula; Ghafula atavunjika, bila njia ya kupona.

16Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake.

17Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia;

18Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu;

19Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.

20Mwanangu, shika maagizo ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako.

21Yafunge hayo katika moyo wako daima; Jivike hayo shingoni mwako.

22Uendapo yatakuongoza, ulalapo yatakulinda, Na uamkapo yatazungumza nawe.

23Maana maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru, Na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima.

24Yakulinde na mwanamke mwovu, asikupate, Na kukuponya na ubembelezi wa mgeni.

25Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake.

26Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani

27Je! Mtu aweza kuua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe?

28Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue?

29Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake; Kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia.

30Watu hawamdharau mwivi, Akiiba ili kujishibisha, iwapo aona njaa;

31Lakini akipatikana, atalipa mara saba; Atatoa mali yote ya nyumba yake.

32Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake.

33Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika.

34Maana wivu ni ghadhabu ya mtu; Wala hatahurumia siku ya kujilipiza kisasi.

35Hatakubali ukombozi uwao wote; Wala hatakuwa radhi, ujapomlipa vitu vingi.