Mithali - Sura ya 8

1Je! Hekima halii? Ufahamu hatoi sauti yake?
2Juu ya mahali palipoinuka karibu na njia, Penye njia panda, ndipo asimamapo.
3Karibu na malango, mahali pa kuingia mjini, Mahali pa kuyaingilia malango anapiga kelele.
4Enyi watu, nawaita ninyi; Na sauti yangu ni kwa wanadamu.
5Enyi wajinga, fahamuni werevu, Nanyi wapumbavu, mpate moyo wa kufahamu.
6Sikieni, maana nitasema yaliyo mazuri, Na kufumbua midomo yangu kutakuwa maadili.
7Maana kinywa changu kitasema kweli, Na uovu ni chukizo kwa midomo yangu.
8Maneno yote ya kinywa changu yana haki; Hapana hata neno lililopotoka au la ukaidi.
9Yote humwelea yule afahamuye, Yote huelekea mbele yao waliopata maarifa.
10Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi.
11Maana hekima ni bora kuliko marijani; Wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo.
12Mimi, hekima, nimefanya werevu kuwa kao langu; Natafuta maarifa na busara.
13Kumcha Bwana ni kuchukia uovu; Kiburi na majivuno, na njia mbovu, Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia.
14Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu, mimi nina nguvu.
15Kwa msaada wangu wafalme humiliki, Na wakuu wanahukumu haki.
16Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia.
17Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.
18Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia.
19Matunda yangu hupita dhahabu, naam, dhahabu safi, Na faida yangu hupita fedha iliyo teule.
20Natembea katika njia ya haki, Katikati ya mapito ya hukumu.
21Niwarithishe mali wale wanipendao, Tena nipate kuzijaza hazina zao.
22Bwana alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale.
23Nalitukuka tokea milele, tangu awali, Kabla haijawako dunia.
24Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, Wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji.
25Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nalizaliwa.
26Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde Wala chanzo cha mavumbi ya dunia;
27Alipozithibitisha mbingu nalikuwako; Alipopiga duara katika uso wa bahari;
28Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari zilipopata nguvu;
29Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza misingi ya nchi;
30Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake;
31Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu.
32Basi, wanangu, nisikilizeni sasa; Maana heri hao wazishikao amri zangu.
33Sikieni mafundisho, mpate hekima, Wala msiikatae.
34Ana heri mtu yule anisikilizaye, Akisubiri sikuzote malangoni pangu, Akingoja penye vizingiti vya milango yangu.
35Maana yeye anionaye mimi aona uzima, Naye atapata kibali kwa Bwana.
36Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, Na wao wanichukiao hupenda mauti.