Mithali - Sura ya 9

1Hekima umeijenga nyumba yake, Amezichonga nguzo zake saba;
2Amechinja nyama zake, umechanganya divai yake, Ameiandalia meza yake pia.
3Amewatuma wajakazi wake, analia, Mahali pa mjini palipoinuka sana,
4Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili,
5Njoo ule mkate wangu, Ukanywe divai niliyoichanganya.
6Enyi wajinga, acheni ujinga, mkaishi, Mkaende katika njia ya ufahamu.
7Amkemeaye mwenye dharau hujipatia fedheha; Amkaripiaye mtu mbaya hujipatia aibu.
8Usimkaripie mwenye dharau, asije akakuchukia; Mkaripie mwenye hekima, naye atakupenda.
9Mwelimishe mwenye hekima, naye atazidi kuwa na hekima; Mfundishe mwenye haki, naye atazidi kuwa na elimu;
10Kumcha Bwana ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu.
11Maana, kwa msaada wangu siku zako zitazidishwa; Na miaka ya maisha yako itaongezwa.
12Kama una hekima, una hekima kwa nafsi yako; Na kama una dharau, utaichukua peke yako.
13Mwanamke mpumbavu hupiga kelele, Ni mjinga, hajui kitu.
14Hukaa mlangoni pa nyumba yake, Juu ya kiti mahali pa mjini palipoinuka,
15Apate kuwaita wapitao njiani, Waendao moja kwa moja katika njia zao.
16Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili,
17Maji yaliyoibiwa ni matamu, Na mkate ulioliwa kwa siri hupendeza.
18Lakini huyo hajui ya kuwa wafu wamo humo; Ya kuwa wageni wake wamo chini kuzimuni.