Zaburi - Sura ya 1

Zaburi - Sura ya 1

1Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.

2Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.

3Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.

4Sivyo walivyo wasio haki; Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.

5Kwa hiyo wasio haki hawatasimama hukumuni, Wala wakosaji katika kusanyiko la wenye haki.

6Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki, Bali njia ya wasio haki itapotea.