Zaburi - Sura ya 10

Zaburi - Sura ya 10

1Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali? Kwani kujificha nyakati za shida?

2Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.

3Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake, Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau.

4Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake Asema, Hatapatiliza. Jumla ya mawazo yake ni, Hakuna Mungu;

5Njia zake ni thabiti kila wakati. Hukumu zako ziko juu asizione, Adui zake wote awafyonya.

6Asema moyoni mwake, Sitaondoshwa, Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni.

7Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,

8Hukaa katika maoteo ya vijiji. Mahali pa siri humwua asiye na hatia, Macho yake humvizia mtu duni.

9Huotea faraghani kama simba pangoni, Huotea amkamate mtu mnyonge. Naam, humkamata mtu mnyonge, Akimkokota wavuni mwake.

10Hujikunyata na kuinama; Watu duni huanguka kwa nguvu zake.

11Asema moyoni mwake, Mungu amesahau, Auficha uso wake, haoni kamwe.

12Bwana, uondoke, Ee Mungu, uuinue mkono wako, Usiwasahau wanyonge.

13Kwani mdhalimu kumdharau Mungu. Akisema moyoni mwake, Hutapatiliza?

14Umeona, maana unaangalia madhara na jeuri, Uyatwae mkononi mwako. Mtu duni hukuachia nafsi yake, Maana umekuwa msaidizi wa yatima.

15Uuvunje mkono wake mdhalimu, Na mbaya, uipatilize dhuluma yake, hata usiione.

16Bwana ndiye Mfalme milele na milele; Mataifa wamepotea kutoka nchi yake.

17Bwana, umeisikia tamaa ya wanyonge, Utaitengeneza mioyo yao, utalitega sikio lako.

18Ili kumhukumu yatima naye aliyeonewa, Binadamu aliye udongo asizidi kudhulumu.