Zaburi - Sura ya 101

Zaburi - Sura ya 101

1Rehema na hukumu nitaziimba, Ee Bwana, nitakuimbia zaburi.

2Nitaiangalia njia ya unyofu; Utakuja kwangu lini? Nitakwenda kwa unyofu wa moyo Ndani ya nyumba yangu.

3Sitaweka mbele ya macho yangu Neno la uovu. Kazi yao waliopotoka naichukia, Haitaambatana nami.

4Moyo wa ukaidi utaondoka kwangu, Lililo ovu sitalijua.

5Amsingiziaye jirani yake kwa siri, Huyo nitamharibu. Mwenye macho ya kiburi na moyo wa majivuno, Huyo sitavumilia naye.

6Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi, Hao wakae nami. Yeye aendaye katika njia kamilifu, Ndiye atakayenitumikia.

7Hatakaa ndani ya nyumba yangu Mtu atendaye hila. Asemaye uongo hatathibitika Mbele ya macho yangu.

8Asubuhi hata asubuhi nitawaharibu Wabaya wote wa nchi. Niwatenge wote watendao uovu Na mji wa Bwana.