Zaburi - Sura ya 103

Zaburi - Sura ya 103

1Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu.

2Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote.

3Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote,

4Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema,

5Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai;

6Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki, Na hukumu kwa wote wanaoonewa.

7Alimjulisha Musa njia zake, Wana wa Israeli matendo yake.

8Bwana amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.

9Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele.

10Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.

11Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao.

12Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.

13Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.

14Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.

15Mwanadamu siku zake zi kama majani; Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo.

16Maana upepo hupita juu yake, kumbe haliko! Na mahali pake hapatalijua tena.

17Bali fadhili za Bwana zina wamchao Tangu milele hata milele, Na haki yake ina wana wa wana;

18Maana, wale walishikao agano lake, Na kuyakumbuka maagizo yake ili wayafanye.

19Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, Na ufalme wake unavitawala vitu vyote.

20Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake.

21Mhimidini Bwana, enyi majeshi yake yote, Ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake.

22Mhimidini Bwana, enyi matendo yake yote, Mahali pote pa milki yake. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.