Zaburi - Sura ya 104
1Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Wewe, Bwana, Mungu wangu, Umejifanya mkuu sana; Umejivika heshima na adhama.
2Umejivika nuru kama vazi; Umezitandika mbingu kama pazia;
3Na kuziweka nguzo za orofa zake majini. Huyafanya mawingu kuwa gari lake, Na kwenda juu ya mabawa ya upepo,
4Huwafanya malaika zake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa moto wa miali.
5Uliiweka nchi juu ya misingi yake, Isitikisike milele.
6Uliifunika kwa vilindi kama kwa vazi, Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima.
7Kwa kukemea kwako yakakimbia, Kwa sauti ya radi yako yakaenda zake kasi,
8Yakapanda milima, yakatelemka mabondeni, Mpaka mahali ulipoyatengenezea.
9Umeweka mpaka yasiupite, Wala yasirudi kuifunikiza nchi.
10Hupeleka chemchemi katika mabonde; Zapita kati ya milima;
11Zamnywesha kila mnyama wa kondeni; Punda mwitu huzima kiu yao.
12Kandokando hukaa ndege wa angani; Kati ya matawi hutoa sauti zao.
13Huinywesha milima toka orofa zake; Nchi imeshiba mazao ya kazi zako.
14Huyameesha majani kwa makundi, Na maboga kwa matumizi ya mwanadamu; Ili atoe chakula katika nchi,
15Na divai imfurahishe mtu moyo wake. Aung'aze uso wake kwa mafuta, Na mkate umburudishe mtu moyo wake.
16Miti ya Bwana nayo imeshiba, Mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
17Ndimo ndege wafanyamo vitundu vyao, Na korongo, misunobari ni nyumba yake.
18Milima mirefu ndiko waliko mbuzi wa mwitu, Na magenge ni kimbilio la wibari.
19Aliufanya mwezi kwa ajili ya nyakati, Jua latambua kuchwa kwake.
20Wewe hufanya giza, kukawa usiku, Ndipo atambaapo kila mnyama wa mwitu.
21Wana-simba hunguruma wakitaka mawindo, Ili kutafuta chakula chao kwa Mungu.
22Jua lachomoza, wanakwenda zao, Na kujilaza mapangoni mwao.
23Mwanadamu atoka kwenda zake kazini, Na kwenye utumishi wake mpaka jioni.
24Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako.
25Bahari iko kule, kubwa na upana, Ndimo mlimo viendavyo visivyohesabika, Viumbe hai vidogo kwa vikubwa.
26Ndimo zipitamo merikebu, Ndimo alimo lewiathani uliyemwumba acheze humo.
27Hao wote wanakungoja Wewe, Uwape chakula chao kwa wakati wake.
28Wewe huwapa, Wao wanakiokota; Wewe waukunjua mkono wako, Wao wanashiba mema;
29Wewe wauficha uso wako, Wao wanafadhaika; Waiondoa pumzi yao, wanakufa, Na kuyarudia mavumbi yao,
30Waipeleka roho yako, wanaumbwa, Nawe waufanya upya uso wa nchi.
31Utukufu wa Bwana na udumu milele; Bwana na ayafurahie matendo yake.
32Aitazama nchi, inatetemeka; Aigusa milima, inatoka moshi.
33Nitamwimbia Bwana maadamu ninaishi; Nitamshangilia Mungu wangu nikiwa hai;
34Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake; Mimi nitamfurahia Bwana.
35Wenye dhambi waangamizwe katika nchi, Watendao ubaya wasiwepo tena. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

Swahili
Italiano (it-IT)
Português do Brasil (pt-BR)
Polski (PL)
Deutsch (Deutschland)
Français (France)
Español (España)
Українська Біблія у перекладі Огієнка
English Bible - 21ST CENTURY KING JAMES (KJ21)