Zaburi - Sura ya 107

Zaburi - Sura ya 107

1Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.

2Na waseme hivi waliokombolewa na Bwana, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi.

3Akawakusanya kutoka nchi zote, Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini.

4Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa.

5Waliona njaa, waliona na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao.

6Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.

7Akawaongoza kwa njia ya kunyoka, Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa.

8Na wamshukuru Bwana, kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.

9Maana hushibisha nafsi yenye shauku, Na nafsi yenye njaa huijaza mema.

10Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma,

11Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye juu.

12Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa wala hakuna msaidizi.

13Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.

14Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akayavunja mafungo yao.

15Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.

16Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma.

17Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao, Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa.

18Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula, Wameyakaribia malango ya mauti.

19Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.

20Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.

21Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.

22Na wamtolee dhabihu za kushukuru, Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba.

23Washukao baharini katika merikebu, Wafanyao kazi yao katika maji mengi,

24Hao huziona kazi za Bwana, Na maajabu yake vilindini.

25Maana husema, akavumisha upepo wa dhoruba, Ukayainua juu mawimbi yake.

26Wapanda mbinguni, watelemka vilindini, Nafsi yao yayeyuka kwa hali mbaya.

27Wayumba-yumba, wapepesuka kama mlevi, Akili zao zote zawapotea.

28Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.

29Huituliza dhoruba, ikawa shwari, Mawimbi yake yakanyamaza.

30Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia Naye huwaleta mpaka bandari waliyoitamani.

31Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.

32Na wamtukuze katika kusanyiko la watu, Na wamhimidi katika baraza ya wazee.

33Amegeuza mito ikawa jangwa, Na chemchemi za maji zikawa nchi ya kiu.

34Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi, Kwa sababu ya ubaya wao walioikaa.

35Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji, Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji.

36Maana amewakalisha huko wenye njaa, Nao wametengeneza mji wa kukaa.

37Wakapanda mbegu katika mashamba, Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake.

38Naye huwabariki wakaongezeka sana, Wala hayapunguzi makundi yao.

39Kisha wakapungua na kudhilika, Kwa kuonewa na mabaya na huzuni.

40Akawamwagia wakuu dharau, Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia.

41Akamweka mhitaji juu mbali na mateso, Akamfanyia jamaa kama kundi la kondoo.

42Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi, Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa.

43Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za Bwana.