Zaburi - Sura ya 111

Zaburi - Sura ya 111

1Haleluya

2Matendo ya Bwana ni makuu, Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo.

3Kazi yake ni heshima na adhama, Na haki yake yakaa milele.

4Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu; Bwana ni mwenye fadhili na rehema.

5Amewapa wamchao chakula; Atalikumbuka agano lake milele.

6Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake, Kwa kuwapa urithi wa mataifa.

7Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu, Maagizo yake yote ni amini,

8Yamethibitika milele na milele, Yamefanywa katika kweli na adili.

9Amewapelekea watu wake ukombozi, Ameamuru agano lake liwe la milele, Jina lake ni takatifu la kuogopwa.

10Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, Wote wafanyao hayo wana akili njema, Sifa zake zakaa milele.