Zaburi - Sura ya 112

Zaburi - Sura ya 112

1Haleluya. Heri mtu yule amchaye Bwana, Apendezwaye sana na maagizo yake.

2Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.

3Nyumbani mwake mna utajiri na mali, Na haki yake yakaa milele.

4Nuru huwazukia wenye adili gizani; Ana fadhili na huruma na haki.

5Heri atendaye fadhili na kukopesha; Atengenezaye mambo yake kwa haki.

6Kwa maana hataondoshwa kamwe; Mwenye haki atakumbukwa milele.

7Hataogopa habari mbaya; Moyo wake u imara ukimtumaini Bwana.

8Moyo wake umethibitika hataogopa, Hata awaone watesi wake wameshindwa.

9Amekirimu, na kuwapa maskini, Haki yake yakaa milele, Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.

10Asiye haki ataona na kusikitika, Atasaga meno yake na kuyeyuka, Tamaa ya wasio haki itapotea.