Zaburi - Sura ya 115

1Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi, Bali ulitukuze jina lako, Kwa ajili ya fadhili zako, Kwa ajili ya uaminifu wako.
2Kwa nini mataifa kusema, Yuko wapi Mungu wao?
3Lakini Mungu wetu yuko mbinguni, Alitakalo lote amelitenda.
4Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu.
5Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni,
6Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu,
7Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake.
8Wazifanyao watafanana nazo, Kila mmoja anayezitumainia.
9Enyi Israeli, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao.
10Enyi mlango wa Haruni, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao.
11Enyi mmchao Bwana, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao.
12Bwana ametukumbuka, Naye atatubariki sisi. Ataubariki mlango wa Israeli, Ataubariki mlango wa Haruni,
13Atawabariki wamchao Bwana, Wadogo kwa wakubwa.
14Bwana na awaongeze ninyi, Ninyi na watoto wenu.
15Na mbarikiwe ninyi na Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.
16Mbingu ni mbingu za Bwana, Bali nchi amewapa wanadamu.
17Sio wafu wamsifuo Bwana, Wala wo wote washukao kwenye kimya;
18Bali sisi tutamhimidi Bwana, Tangu leo na hata milele.