Zaburi - Sura ya 118

1Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.
2Israeli na aseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
3Mlango wa Haruni na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
4Wamchao Bwana na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
5Katika shida yangu nalimwita Bwana; Bwana akanijibu akaniweka panapo nafasi.
6Bwana yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?
7Bwana yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa.
8Ni heri kumkimbilia Bwana Kuliko kuwatumainia wanadamu.
9Ni heri kumkimbilia Bwana. Kuliko kuwatumainia wakuu.
10Mataifa yote walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
11Walinizunguka, naam, walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
12Walinizunguka kama nyuki, Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
13Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini Bwana akanisaidia.
14Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, Naye amekuwa wokovu wangu.
15Sauti ya furaha na wokovu Imo hemani mwao wenye haki; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
16Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
17Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya Bwana.
18Bwana ameniadhibu sana, Lakini hakuniacha nife.
19Nifungulieni malango ya haki, Nitaingia na kumshukuru Bwana.
20Lango hili ni la Bwana, Wenye haki ndio watakaoliingia.
21Nitakushukuru kwa maana umenijibu, Nawe umekuwa wokovu wangu.
22Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
23Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu.
24Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.
25Ee Bwana, utuokoe, twakusihi; Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi.
26Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana; Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.
27Bwana ndiye aliye Mungu, Naye ndiye aliyetupa nuru. Ifungeni dhabihu kwa kamba Pembeni mwa madhabahu.
28Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru, Ndiwe Mungu wangu, nami nitakutukuza.
29Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.