Zaburi - Sura ya 119

Zaburi - Sura ya 119

1Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana.

2Heri wazitiio shuhuda zake, Wamtafutao kwa moyo wote.

3Naam, hawakutenda ubatili, Wamekwenda katika njia zake.

4Wewe umetuamuru mausia yako, Ili sisi tuyatii sana.

5Ningependa njia zangu ziwe thabiti, Nizitii amri zako.

6Ndipo mimi sitaaibika, Nikiyaangalia maagizo yako yote.

7Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo, Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako

8Nitazitii amri zako, Usiniache kabisa

9Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako.

10Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.

11Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.

12Ee Bwana, umehimidiwa, Unifundishe amri zako.

13Kwa midomo yangu nimezisimulia Hukumu zote za kinywa chako.

14Nimeifurahia njia ya shuhuda zako Kana kwamba ni mali mengi.

15Nitayatafakari mausia yako, Nami nitaziangalia njia zako.

16Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako.

17Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.

18Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako.

19Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako.

20Roho yangu imepondeka kwa kutamani Hukumu zako kila wakati.

21Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako.

22Uniondolee laumu na dharau, Kwa maana nimezishika shuhuda zako.

23Wakuu nao waliketi wakaninena, Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako.

24Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu, Na washauri wangu.

25Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako.

26Nalizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako.

27Unifahamishe njia ya mausia yako, Nami nitayatafakari maajabu yako.

28Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito, Unitie nguvu sawasawa na neno lako.

29Uniondolee njia ya uongo, Unineemeshe kwa sheria yako.

30Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu.

31Nimeambatana na shuhuda zako, Ee Bwana, usiniaibishe.

32Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako, Utakaponikunjua moyo wangu.

33Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako, Nami nitaishika hata mwisho.

34Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.

35Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Kwa maana nimependezwa nayo.

36Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako, Wala usiielekee tamaa.

37Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako.

38Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako, Inayohusu kicho chako.

39Uniondolee laumu niiogopayo, Maana hukumu zako ni njema.

40Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako.

41Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako.

42Nami nitamjibu neno anilaumuye, Kwa maana nalitumainia neno lako.

43Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, Maana nimezingojea hukumu zako.

44Nami nitaitii sheria yako daima, Naam, milele na milele.

45Nami nitakwenda panapo nafasi, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako.

46Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu.

47Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda.

48Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako.

49Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, Kwa sababu umenitumainisha.

50Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imenihuisha.

51Wenye kiburi wamenidharau mno, Sikujiepusha na sheria zako.

52Nimezikumbuka hukumu zako za kale, Ee Bwana, nikajifariji.

53Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki, Waiachao sheria yako.

54Amri zako zimekuwa nyimbo zangu, Katika nyumba ya ugeni wangu.

55Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako, Ee Bwana, nikaitii sheria yako.

56Hayo ndiyo niliyokuwa nayo, Kwa sababu nimeyashika mausia yako.

57Bwana ndiye aliye fungu langu, Nimesema kwamba nitayatii maneno yake.

58Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote, Unifadhili sawasawa na ahadi yako.

59Nalizitafakari njia zangu, Na miguu yangu nalizielekezea shuhuda zako.

60Nalifanya haraka wala sikukawia, Kuyatii maagizo yako.

61Kamba za wasio haki zimenifunga, Sikuisahau sheria yako.

62Katikati ya usiku nitaamka nikushukuru, Kwa sababu ya hukumu zako za haki.

63Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao, Na wale wayatiio mausia yako.

64Bwana, dunia imejaa fadhili zako, Unifundishe amri zako.

65Umemtendea mema mtumishi wako, Ee Bwana, sawasawa na neno lako.

66Unifundishe akili na maarifa, Maana nimeyaamini maagizo yako.

67Kabla sijateswa mimi nalipotea, Lakini sasa nimelitii neno lako.

68Wewe U mwema na mtenda mema, Unifundishe amri zako.

69Wenye kiburi wamenizulia uongo, Kwa moyo wangu wote nitayashika mausia yako.

70Mioyo yao imenenepa kama shahamu, Mimi nimeifurahia sheria yako.

71Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, Nipate kujifunza amri zako.

72Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.

73Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako.

74Wakuchao na wanione na kufurahi, Kwa sababu nimelingojea neno lako.

75Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki, Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa.

76Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu, Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako.

77Rehema zako zinijie nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu.

78Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo, Mimi nitayatafakari mausia yako.

79Wakuchao na wanirudie, Nao watazijua shuhuda zako.

80Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako, Nisije mimi nikaaibika.

81Nafsi yangu imefifia kwa kuutamani wokovu wako, Nimelingojea neno lako.

82Macho yangu yamefifia kwa kuitazamia ahadi yako, Nisemapo, Lini utakaponifariji?

83Maana nimekuwa kama kiriba katika moshi, Sikuzisahau amri zako.

84Siku za mtumishi wako ni ngapi, Lini utakapowahukumu wale wanaonifuatia?

85Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, Ambao hawaifuati sheria yako.

86Maagizo yako yote ni amini, Wananifuatia bure, unisaidie.

87Walikuwa karibu na kunikomesha katika nchi, Lakini sikuyaacha mausia yako.

88Unihuishe kwa fadhili zako, Nami nitazishika shuhuda za kinywa chako.

89Ee Bwana, neno lako lasimama Imara mbinguni hata milele.

90Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa.

91Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako.

92Kama sheria yako isingalikuwa furaha yangu, Hapo ningalipotea katika taabu zangu.

93Hata milele sitayasahau maagizo yako, Maana kwa hayo umenihuisha.

94Mimi ni wako, uniokoe, Kwa maana nimejifunza mausia yako.

95Wasio haki wameniotea ili kunipoteza, Nitazitafakari shuhuda zako.

96Nimeona ukamilifu wote kuwa na mwisho, Bali agizo lako ni pana mno.

97Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.

98Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu, Kwa maana ninayo sikuzote.

99Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote, Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo.

100Ninao ufahamu kuliko wazee, Kwa kuwa nimeyashika mausia yako.

101Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya, Ili nilitii neno lako.

102Sikujiepusha na hukumu zako, Maana Wewe mwenyewe umenifundisha.

103Mausia yako ni matamu sana kwangu, Kupita asali kinywani mwangu.

104Kwa mausia yako najipatia ufahamu, Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo.

105Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.

106Nimeapa nami nitaifikiliza, Kuzishika hukumu za haki yako.

107Nimeteswa mno; Ee Bwana, unihuishe sawasawa na neno lako.

108Ee Bwana, uziridhie sadaka za kinywa changu, Na kunifundisha hukumu zako.

109Nafsi yangu imo mkononi mwangu daima, Lakini sheria yako sikuisahau.

110Watendao uovu wamenitegea mtego, Lakini sikuikosa njia ya mausia yako.

111Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele, Maana ndizo changamko la moyo wangu.

112Nimeuelekeza moyo wangu nizitende amri zako, Daima, naam, hata milele.

113Watu wa kusita-sita nawachukia, Lakini sheria yako naipenda.

114Ndiwe sitara yangu na ngao yangu, Neno lako nimelingojea.

115Enyi watenda mabaya, ondokeni kwangu, Niyashike maagizo ya Mungu wangu.

116Unitegemeze sawasawa na ahadi yako, nikaishi, Wala usiniache niyaaibikie matumaini yangu.

117Unisaidie nami nitakuwa salama, Nami nitaziangalia amri zako daima.

118Umewakataa wote wazikosao amri zako, Kwa maana hila zao ni uongo.

119Wabaya wa nchi pia umewaondoa kama takataka, Ndiyo maana nimezipenda shuhuda zako.

120Mwili wangu unatetemeka kwa kukucha Wewe, Nami ninaziogopa hukumu zako.

121Nimefanya hukumu na haki, Usiniache mikononi mwao wanaonionea.

122Uwe mdhamini wa mtumishi wako, apate mema, Wenye kiburi wasinionee.

123Macho yangu yamefifia kwa kuutamani wokovu wako, Na ahadi ya haki yako.

124Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako, Na amri zako unifundishe.

125Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe, Nipate kuzijua shuhuda zako.

126Wakati umewadia Bwana atende kazi; Kwa kuwa wameitangua sheria yako.

127Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako, Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi.

128Maana nayaona mausia yako yote kuwa ya adili, Kila njia ya uongo naichukia.

129Shuhuda zako ni za ajabu, Ndiyo maana roho yangu imezishika.

130Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga.

131Nalifunua kinywa changu nikatweta, Maana naliyatamani maagizo yako.

132Unigeukie, unirehemu mimi, Kama iwahusuvyo walipendao jina lako.

133Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, Uovu usije ukanimiliki.

134Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu, Nipate kuyashika mausia yako.

135Umwangazie mtumishi wako uso wako, Na kunifundisha amri zako.

136Macho yangu yachuruzika mito ya maji, Kwa sababu hawaitii sheria yako.

137Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki, Na hukumu zako ni za adili.

138Umeziagiza shuhuda zako kwa haki, Na kwa uaminifu mwingi.

139Juhudi yangu imeniangamiza, Maana watesi wangu wameyasahau maneno yako.

140Neno lako limesafika sana, Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda.

141Mimi ni mdogo, nadharauliwa, Lakini siyasahau mausia yako.

142Haki yako ni haki ya milele, Na sheria yako ni kweli.

143Taabu na dhiki zimenipata, Maagizo yako ni furaha yangu.

144Haki ya shuhuda zako ni ya milele, Unifahamishe, nami nitaishi.

145Nimeita kwa moyo wangu wote; Ee Bwana, uitike; Nitazishika amri zako.

146Nimekuita Wewe, uniokoe, Nami nitazishika shuhuda zako.

147Kutangulia mapambazuko naliomba msaada, Naliyangojea maneno yako kwa tumaini.

148Macho yangu yalitangulia makesha ya usiku, Ili kuitafakari ahadi yako.

149Uisikie sauti yangu sawasawa na fadhili zako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na hukumu yako.

150Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki, Wamekwenda mbali na sheria yako.

151Ee Bwana, Wewe U karibu, Na maagizo yako yote ni kweli.

152Tokea zamani nimejua kwa shuhuda zako, Ya kuwa umeziweka zikae milele.

153Uyaangalie mateso yangu, uniokoe, Maana sikuisahau sheria yako.

154Unitetee na kunikomboa, Unihuishe sawasawa na ahadi yako.

155Wokovu u mbali na wasio haki, Kwa maana hawajifunzi amri zako.

156Ee Bwana, rehema zako ni nyingi, Unihuishe sawasawa na hukumu zako.

157Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi, Lakini sikujiepusha na shuhuda zako.

158Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa, Kwa sababu hawakulitii neno lako.

159Uangalie niyapendavyo mausia yako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na fadhili zako.

160Jumla ya neno lako ni kweli, Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele.

161Wakuu wameniudhi bure, Ila moyo wangu unayahofia maneno yako.

162Naifurahia ahadi yako, Kama apataye mateka mengi.

163Nimeuchukia uongo, umenikirihi, Sheria yako nimeipenda.

164Mara saba kila siku nakusifu, Kwa sababu ya hukumu za haki yako.

165Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza.

166Ee Bwana, nimeungojea wokovu wako, Na maagizo yako nimeyatenda.

167Nafsi yangu imezishika shuhuda zako, Nami nazipenda mno.

168Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako, Maana njia zangu zote zi mbele zako.

169Ee Bwana, kilio changu na kikukaribie, Unifahamishe sawasawa na neno lako.

170Dua yangu na ifike mbele zako, Uniponye sawasawa na ahadi yako.

171Midomo yangu na itoe sifa, Kwa kuwa unanifundisha mausia yako.

172Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako, Maana maagizo yako yote ni ya haki.

173Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, Maana nimeyachagua mausia yako.

174Ee Bwana, nimeutamani wokovu wako, Na sheria yako ndiyo furaha yangu.

175Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu, Na hukumu zako zinisaidie.

176Nimetanga-tanga kama kondoo aliyepotea; Umtafute mtumishi wako; Kwa maana sikuyasahau maagizo yako.