Zaburi - Sura ya 132
1Bwana, umkumbukie Daudi Taabu zake zote alizotaabika.
2Ndiye aliyemwapia Bwana, Akaweka nadhiri kwa Shujaa wa Yakobo.
3Sitaingia hemani mwa nyumba yangu, Wala sitapanda matandiko ya kitanda changu;
4Sitaacha macho yangu kuwa na usingizi, Wala kope zangu kusinzia;
5Hata nitakapompatia Bwana mahali, Na Shujaa wa Yakobo maskani.
6Tazama, tulisikia habari zake katika Efrata, Katika konde la Yearimu tuliiona.
7Na tuingie katika maskani yake, Tusujudu penye kiti cha kuwekea miguu yake.
8Ee Bwana, uinuke, uende kwenye raha yako, Wewe na sanduku la nguvu zako.
9Makuhani wako na wavikwe haki, Watauwa wako na washangilie.
10Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako, Usiurudishe nyuma uso wa masihi
11Bwana amemwapia Daudi neno la kweli, Hatarudi nyuma akalihalifu, Baadhi ya wazao wa mwili wako Nitawaweka katika kiti chako cha enzi.
12Wanao wakiyashika maagano yangu, Na shuhuda nitakazowafundisha; Watoto wao nao wataketi Katika kiti chako cha enzi milele.
13Kwa kuwa Bwana ameichagua Sayuni, Ameitamani akae ndani yake.
14Hapo ndipo mahali pangu pa raha milele, Hapo nitakaa kwa maana nimepatamani.
15Hakika nitavibariki vyakula vyake Wahitaji wake nitawashibisha chakula.
16Na makuhani wake nitawavika wokovu, Na watauwa wake watashangilia.
17Hapo nitamchipushia Daudi pembe, Na taa nimemtengenezea masihi
18Adui zake nitawavika aibu, Bali juu yake taji yake itasitawi.