Zaburi - Sura ya 139

1Ee Bwana, umenichunguza na kunijua.
2Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
3Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote.
4Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana.
5Umenizingira nyuma na mbele, Ukaniwekea mkono wako.
6Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi, Hayadirikiki, siwezi kuyafikia.
7Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako?
8Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.
9Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari;
10Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika.
11Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku;
12Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa.
13Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
14Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana,
15Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi;
16Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado.
17Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake!
18Kama ningezihesabu ni nyingi kuliko mchanga; Niamkapo nikali pamoja nawe.
19Ee Mungu, laiti ungewafisha waovu! Enyi watu wa damu, ondokeni kwangu;
20Kwa maana wakuasi kwa ubaya, Adui zako wakutaja jina lako bure.
21Je! Bwana nisiwachukie wanaokuchukia? Nisikirihike nao wakuasio?
22Nawachukia kwa ukomo wa chuki, Wamekuwa adui kwangu.
23Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu;
24Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele.