Zaburi - Sura ya 140

Zaburi - Sura ya 140

1Ee Bwana, uniokoe na mtu mbaya, Unihifadhi na mtu wa jeuri.

2Waliowaza mabaya mioyoni mwao, Kila siku huondokesha vita.

3Wamenoa ndimi zao kama nyoka, Sumu ya fira i chini ya midomo yao.

4Ee Bwana, unilinde na mikono ya mtu asiye haki; Unihifadhi na mtu wa jeuri; Waliowaza kuzipotosha hatua zangu.

5Wenye kiburi wamenifichia mtego na kamba; Wametandika wavu kando ya njia; Wameniwekea matanzi.

6Nimemwambia Bwana, Ndiwe Mungu wangu; Ee Bwana, uisikie sauti ya dua zangu.

7Ee MUNGU Bwana, nguvu za wokovu wangu, Umenifunika kichwa changu siku ya vita.

8Ee Bwana, usimpe asiye haki tamaa zake, Usiifanikishe hila yake, wasije wakajiinua.

9Nao wainuapo vichwa watu wanaonizunguka, Madhara ya midomo yao yawafunike.

10Makaa ya moto yawaangukie, watupwe motoni, Na katika mashimo, wasipate kusimama tena.

11Msingiziaji hatawekwa imara katika nchi, Mtu wa jeuri, uovu humwinda kumwangamiza.

12Najua ya kuwa Bwana atamfanyia mnyonge hukumu, Na wahitaji haki yao.

13Hakika wenye haki watalishukuru jina lako, Wenye adili watakaa mahali ulipo Wewe.