Zaburi - Sura ya 141

Zaburi - Sura ya 141

1Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo.

2Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.

3Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.

4Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya, Nisiyazoelee matendo yasiyofaa, Pamoja na watu watendao maovu; Wala nisile vyakula vyao vya anasa.

5Mwenye haki na anipige, itakuwa fadhili; Anikemee, itakuwa kama mafuta kichwani; Kichwa changu kisikatae, Maana siachi kusali kati ya mabaya yao.

6Makadhi wao wakiangushwa kando ya genge, Watayasikia maneno yangu, maana ni matamu.

7Kama kupasua kuni na kuzichanja juu ya nchi, Ndivyo ilivyo mifupa yetu mdomoni pa kuzimu.

8Macho yangu yanakuelekea Wewe, MUNGU Bwana, Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu.

9Unilinde na mtego walionitegea, Na matanzi yao watendao maovu.

10Wabaya na waanguke katika nyavu zao wenyewe, Pindi mimi ninapopita salama.