Zaburi - Sura ya 142

Zaburi - Sura ya 142

1Kwa sauti yangu nitamlilia Bwana, Kwa sauti yangu nitamwomba Bwana dua.

2Nitafunua mbele zake malalamiko yangu, Shida yangu nitaitangaza mbele zake.

3Nilipozimia roho uliyajua mapito yangu; Katika njia niendayo wamenifichia mtego.

4Utazame mkono wa kuume ukaone, Kwa maana sina mtu anijuaye. Makimbilio yamenipotea, Hakuna wa kunitunza roho.

5Bwana, nimekuita nikasema, Ndiwe kimbilio langu, Fungu langu katika nchi ya walio hai.

6Ukisikilize kilio changu, Kwa maana nimedhilika sana. Uniponye nao wanaonifuatia, Kwa maana wao ni hodari kuliko mimi.

7Uitoe nafsi yangu kifungoni. Nipate kulishukuru jina lako. Wenye haki watanizunguka, Kwa kuwa Wewe unanikirimu.