Zaburi - Sura ya 143

Zaburi - Sura ya 143

1Ee Bwana, uisikie sala yangu, uzisikilize dua zangu, Kwa uaminifu wako unijibu kwa haki yako.

2Wala usimhukumu mtumishi wako, Maana kwako hakuna aliye hai mwenye haki.

3Maana adui ameifuatia nafsi yangu, Ameutupa chini uzima wangu. Amenikalisha mahali penye giza, Kama watu waliokufa zamani.

4Na roho yangu imezimia ndani yangu, Moyo wangu ndani yangu umesituka.

5Nimezikumbuka siku za kale, Nimeyatafakari matendo yako yote, Naziwaza kazi za mikono yako.

6Nakunyoshea mikono yangu; Nafsi yangu inakuonea kiu kama nchi kame.

7Ee Bwana, unijibu hima, roho yangu imelegea; Usinifiche uso wako, Nisifanane nao washukao shimoni

8Unifanye kusikia fadhili zako asubuhi, Kwa maana nimekutumaini Wewe. Unijulishe njia nitakayoiendea, Kwa maana nakuinulia nafsi yangu.

9Ee Bwana, uniponye na adui zangu; Nimekukimbilia Wewe, unifiche.

10Unifundishe kuyatenda mapenzi yako, Kwa maana ndiwe Mungu wangu; Roho yako mwema aniongoze kwenye nchi sawa,

11Ee Bwana, unihuishe kwa ajili ya jina lako, Kwa haki yako unitoe roho yangu taabuni;

12Kwa fadhili zako utawakatilia mbali adui zangu; Na kuwaangamiza wote wanitesao nafsi, Kwa maana mimi ni mtumishi wako.