Zaburi - Sura ya 144

Zaburi - Sura ya 144

1Na ahimidiwe Bwana, mwamba wangu, Anifundishaye mikono yangu vita, Vidole vyangu kupigana.

2Mhisani wangu na boma langu, Ngome yangu na mwokozi wangu, Ngao yangu niliyemkimbilia, Huwatiisha watu wangu chini yangu.

3Ee Bwana, mtu ni kitu gani hata umjue? Na binadamu hata umwangalie?

4Binadamu amefanana na ubatili, Siku zake ni kama kivuli kipitacho.

5Bwana, uziinamishe mbingu zako, ushuke, Uiguse milima nayo itatoka moshi.

6Utupe umeme, uwatawanye, Uipige mishale yako, uwafadhaishe.

7Uinyoshe mikono yako toka juu, uniponye, Unitoe katika maji mengi, katika mkono wa wageni.

8Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo.

9Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia.

10Awapaye wafalme wokovu, Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu.

11Uniponye, unitoe, Katika mkono wa wageni. Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo.

12Wana wetu na wawe kama miche Waliokua ujanani. Binti zetu kama nguzo za pembeni Zilizonakishwa kwa kupamba hekalu.

13Ghala zetu na zijae Zenye akiba za jinsi zote. Kondoo zetu na wazae Elfu na makumi elfu mashambani mwetu.

14Ng'ombe zetu na wachukue mizigo, Kusiwe na kushambuliwa. Wala kusiwe na kuhamishwa, Wala malalamiko katika njia zetu.

15Heri watu wenye hali hiyo, Heri watu wenye Bwana kuwa Mungu wao.