Zaburi - Sura ya 145

1Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza, Nitalihimidi jina lako milele na milele.
2Kila siku nitakuhimidi, Nitalisifu jina lako milele na milele.
3Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana, Wala ukuu wake hautambulikani.
4Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako, Kitayatangaza matendo yako makuu.
5Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako, Na matendo yako yote ya ajabu.
6Watu watayataja matendo yako ya kutisha, Nami nitausimulia ukuu wako.
7Watalihubiri kumbukumbu la wema wako mkuu. Wataiimba haki yako.
8Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,
9Bwana ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
10Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
11Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kuuhadithia uweza wako.
12Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu, Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.
13Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote, Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
14Bwana huwategemeza wote waangukao, Huwainua wote walioinama chini.
15Macho ya watu wote yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake.
16Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.
17Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
18Bwana yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu.
19Atawafanyia wamchao matakwa yao, Naye atakisikia kilio chao na kuwaokoa.
20Bwana huwahifadhi wote wampendao, Na wote wasio haki atawaangamiza.
21Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana; Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu milele na milele.