Zaburi - Sura ya 147

Zaburi - Sura ya 147

1Haleluya. Msifuni Bwana; Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu, Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri.

2Bwana ndiye aijengaye Yerusalemu, Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli.

3Huwaponya waliopondeka moyo, Na kuziganga jeraha zao.

4Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina.

5Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mpaka.

6Bwana huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri.

7Mwimbieni Bwana kwa kushukuru, Mwimbieni Mungu wetu kwa kinubi.

8Huzifunika mbingu kwa mawingu, Huitengenezea nchi mvua, Na kuyameesha majani milimani.

9Humpa mnyama chakula chake, Wana-kunguru waliao.

10Hapendezwi na nguvu za farasi, Wala hairidhii miguu ya mtu.

11Bwana huwaridhia wao wamchao, Na kuzitarajia fadhili zake.

12Msifu Bwana, Ee Yerusalemu; Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.

13Maana ameyakaza mapingo ya malango yako, Amewabariki wanao ndani yako.

14Ndiye afanyaye amani mipakani mwako, Akushibishaye kwa unono wa ngano.

15Huipeleka amri yake juu ya nchi, Neno lake lapiga mbio sana.

16Ndiye atoaye theluji kama sufu, Huimwaga barafu yake kama majivu,

17Hutupa mvua ya mawe kama makombo, Mbele ya baridi yake ni nani awezaye kusimama?

18Hulituma neno lake na kuviyeyusha, Huuvumisha upepo wake, maji yakatiririka.

19Humhubiri Yakobo neno lake, Na Israeli amri zake na hukumu zake.

20Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo, Wala hukumu zake hawakuzijua. Haleluya.