Zaburi - Sura ya 148

Zaburi - Sura ya 148

1Haleluya. Msifuni Bwana kutoka mbinguni; Msifuni katika mahali palipo juu.

2Msifuni, enyi malaika wake wote; Msifuni, majeshi yake yote.

3Msifuni, jua na mwezi; Msifuni, nyota zote zenye mwanga.

4Msifuni, enyi mbingu za mbingu, Nanyi maji mlioko juu ya mbingu.

5Na vilisifu jina la Bwana, Kwa maana aliamuru, vikaumbwa.

6Amevithibitisha hata milele na milele, Ametoa amri wala haitapita.

7Msifuni Bwana kutoka nchi, Enyi nyangumi na vilindi vyote.

8Moto na mvua ya mawe, theluji na mvuke, Upepo wa dhoruba ulitendao neno lake.

9Milima na vilima vyote, Miti yenye matunda na mierezi yote.

10Hayawani, na wanyama wafugwao, Vitambaavyo, na ndege wenye mbawa.

11Wafalme wa dunia, na watu wote, Wakuu, na makadhi wote wa dunia.

12Vijana waume, na wanawali, Wazee, na watoto;

13Na walisifu jina la Bwana, Maana jina lake peke yake limetukuka; Adhama yake i juu ya nchi na mbingu.

14Naye amewainulia watu wake pembe, Sifa za watauwa wake wote; Wana wa Israeli, watu walio karibu naye. Haleluya.