Zaburi - Sura ya 17

Zaburi - Sura ya 17

1Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila.

2Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili.

3Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, Umenihakikisha usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose,

4Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri.

5Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa.

6Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu.

7Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kuume Uwaokoe nao wanaowaondokea.

8Unilinde kama mboni ya jicho, Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;

9Wasinione wasio haki wanaonionea, Adui za roho yangu wanaonizunguka.

10Wameukaza moyo wako, Kwa vinywa vyao hutoa majivuno.

11Sasa wametuzunguka hatua zetu, Na kuyakaza macho yao watuangushe chini.

12Kama mfano wa simba atakaye kurarua, Kama mwana-simba aoteaye katika maoteo yake.

13Ee Bwana, usimame, umkabili, umwinamishe, Kwa upanga wako uniokoe nafsi na mtu mbaya.

14Ee Bwana, kwa mkono wako uniokoe na watu, Watu wa dunia hii ambao fungu lao li katika maisha haya. Matumbo yao wayajaza kwa hazina yako, Hushiba wana, huwaachia watoto wao akiba zao,

15Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.