Zaburi - Sura ya 19

Zaburi - Sura ya 19

1Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.

2Mchana husemezana na mchana, Usiku hutolea usiku maarifa.

3Hakuna lugha wala maneno, Sauti yao haisikilikani.

4Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. Katika hizo ameliwekea jua hema,

5Kama bwana arusi akitoka chumbani mwake, Lafurahi kama mtu aliye hodari Kwenda mbio katika njia yake.

6Kutoka kwake lautoka mwisho wa mbingu, Na kuzunguka kwake hata miisho yake, Wala kwa hari yake Hakuna kitu kilichositirika.

7Sheria ya Bwana ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima.

8Maagizo ya Bwana ni ya adili, Huufurahisha moyo. Amri ya Bwana ni safi, Huyatia macho nuru.

9Kicho cha Bwana ni kitakatifu, Kinadumu milele. Hukumu za Bwana ni kweli, Zina haki kabisa.

10Ni za kutamanika kuliko dhahabu, Kuliko wingi wa dhahabu safi. Nazo ni tamu kuliko asali, Kuliko sega la asali.

11Tena mtumishi wako huonywa kwazo, Katika kuzishika kuna thawabu nyingi.

12Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri.

13Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi, Yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, Nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa.

14Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.