Zaburi - Sura ya 22

1Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu?
2Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha.
3Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli.
4Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa.
5Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike.
6Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu.
7Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;
8Husema, Umtegemee Bwana; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye.
9Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu.
10Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu.
11Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi.
12Mafahali wengi wamenizunguka, Walio hodari wa Bashani wamenisonga;
13Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma.
14Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu.
15Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti
16Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenizua mikono na miguu.
17Naweza kuihesabu mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho.
18Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura.
19Nawe, Bwana, usiwe mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia.
20Uniponye nafsi yangu na upanga, Mpenzi wangu na nguvu za mbwa.
21Kinywani mwa simba uniokoe; Naam, toka pembe za nyati umenijibu.
22Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, Katikati ya kusanyiko nitakusifu.
23Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni, Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni, Mcheni, enyi nyote mlio wazao wa Israeli.
24Maana hakulidharau teso la mteswa, Wala hakuchukizwa nalo; Wala hakumficha uso wake, Bali alipomlilia akamsikia.
25Kwako zinatoka sifa zangu Katika kusanyiko kubwa. Nitaziondoa nadhiri zangu Mbele yao wamchao.
26Wapole watakula na kushiba, Wamtafutao Bwana watamsifu; Mioyo yenu na iishi milele.
27Miisho yote ya dunia itakumbuka, Na watu watamrejea Bwana; Jamaa zote za mataifa watamsujudia.
28Maana ufalme una Bwana, Naye ndiye awatawalaye mataifa.
29Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu, Humwinamia wote washukao mavumbini; Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,
30Wazao wake watamtumikia. Zitasimuliwa habari za Bwana, Kwa kizazi kitakachokuja,
31Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake, Ya kwamba ndiye aliyeyafanya.