Zaburi - Sura ya 23

1Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.
2Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
3Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
4Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.
5Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika.
6Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.