Zaburi - Sura ya 24

1Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake.
2Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari, Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
3Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
4Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili, Wala hakuapa kwa hila.
5Atapokea baraka kwa Bwana, Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
6Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao, Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo.
7Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Inukeni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia.
8Ni nani Mfalme wa utukufu? Bwana mwenye nguvu, hodari, Bwana hodari wa vita.
9Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Naam, viinueni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia.
10Ni nani huyu Mfalme wa utukufu? Bwana wa majeshi, Yeye ndiye Mfalme wa utukufu.