Zaburi - Sura ya 25

Zaburi - Sura ya 25

1Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu,

2Ee Mungu wangu, Nimekutumaini Wewe, nisiaibike, Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda.

3Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja; Wataaibika watendao uhaini bila sababu.

4Ee Bwana, unijulishe njia zako, Unifundishe mapito yako,

5Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha. Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu, Nakungoja Wewe mchana kutwa.

6Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako, Maana zimekuwako tokea zamani.

7Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu, Wala maasi yangu. Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako, Ee Bwana kwa ajili ya wema wako.

8Bwana yu mwema, mwenye adili, Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.

9Wenye upole atawaongoza katika hukumu, Wenye upole atawafundisha njia yake.

10Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli, Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.

11Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako, Unisamehe uovu wangu, maana ni mwingi.

12Ni nani amchaye Bwana? Atamfundisha katika njia anayoichagua.

13Nafsi yake itakaa hali ya kufanikiwa; Wazao wake watairithi nchi.

14Siri ya Bwana iko kwao wamchao, Naye atawajulisha agano lake.

15Macho yangu humwelekea Bwana daima, Naye atanitoa miguu yangu katika wavu.

16Uniangalie na kunifadhili, Maana mimi ni mkiwa na mteswa.

17Katika shida za moyo wangu unifanyie nafasi, Na kunitoa katika dhiki zangu.

18Utazame teso langu na taabu yangu; Unisamehe dhambi zangu zote.

19Uwatazame adui zangu, maana ni wengi, Wananichukia kwa machukio ya ukali.

20Unilinde nafsi yangu na kuniponya, Nisiaibike, maana nakukimbilia Wewe.

21Ukamilifu na unyofu zinihifadhi, Maana nakungoja Wewe.

22Ee Mungu, umkomboe Israeli, Katika taabu zake zote.