Zaburi - Sura ya 27

Zaburi - Sura ya 27

1Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?

2Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka.

3Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.

4Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake.

5Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba.

6Na sasa kichwa changu kitainuka Juu ya adui zangu wanaonizunguka. Nami nitatoa dhabihu za shangwe hemani mwake; Nitaimba, naam, nitamhimidi Bwana.

7Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu.

8Uliposema, Nitafuteni uso wangu, Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta.

9Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu.

10Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali Bwana atanikaribisha kwake.

11Ee Bwana, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea;

12Usinitie katika nia ya watesi wangu; Maana mashahidi wa uongo wameniondokea, Nao watoao jeuri kama pumzi.

13Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana Katika nchi ya walio hai.

14Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.