Zaburi - Sura ya 28

Zaburi - Sura ya 28

1Ee Bwana, nitakuita Wewe, mwamba wangu, Usiwe kwangu kama kiziwi. Nisije nikafanana nao washukao shimoni, Ikiwa umeninyamalia.

2Uisikie sauti ya dua yangu nikuombapo, Nikipainulia patakatifu pako mikono yangu.

3Usinikokote pamoja na wasio haki, Wala pamoja na watenda maovu. Wawaambiao jirani zao maneno ya amani, Lakini mioyoni mwao mna madhara.

4Uwape sawasawa na vitendo vyao, Na kwa kadiri ya ubaya wa kufanya kwao, Uwape sawasawa na kazi ya mikono yao, Uwalipe stahili zao.

5Maana hawazifahamu kazi za Bwana, Wala matendo ya mikono yake. Atawavunja wala hatawajenga;

6Na ahimidiwe Bwana. Maana ameisikia sauti ya dua yangu;

7Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu. Moyo wangu umemtumaini, Nami nimesaidiwa; Basi, moyo wangu unashangilia, Na kwa wimbo wangu nitamshukuru.

8Bwana ni nguvu za watu wake, Naye ni ngome ya wokovu kwa masihi

9Uwaokoe watu wako, uubariki urithi wako, Uwachunge, uwachukue milele.