Zaburi - Sura ya 30

Zaburi - Sura ya 30

1Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua, Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.

2Ee Bwana, Mungu wangu, Nalikulilia ukaniponya.

3Umeniinua nafsi yangu, Ee Bwana, kutoka kuzimu. Umenihuisha na kunitoa Miongoni mwao washukao shimoni.

4Mwimbieni Bwana zaburi, Enyi watauwa wake. Na kufanya shukrani. Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.

5Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo, Katika radhi yake mna uhai. Huenda kilio huja kukaa usiku, Lakini asubuhi huwa furaha.

6Nami nilipofanikiwa nalisema, Sitaondoshwa milele.

7Bwana, kwa radhi yako Wewe uliuimarisha mlima wangu. Uliuficha uso wako, Nami nikafadhaika.

8Ee Bwana, nalikulilia Wewe, Naam, kwa Bwana naliomba dua.

9Mna faida gani katika damu yangu Nishukapo shimoni? Mavumbi yatakusifu? Yataitangaza kweli yako?

10Ee Bwana, usikie, unirehemu, Bwana, uwe msaidizi wangu.

11Uligeuza matanga yangu kuwa machezo; Ulinivua gunia, ukanivika furaha.

12Ili utukufu wangu ukusifu, Wala usinyamaze. Ee Bwana, Mungu wangu, Nitakushukuru milele.