Zaburi - Sura ya 31

Zaburi - Sura ya 31

1Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye,

2Unitegee sikio lako, uniokoe hima. Uwe kwangu mwamba wa nguvu, Nyumba yenye maboma ya kuniokoa.

3Ndiwe genge langu na ngome yangu; Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge.

4Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri, Maana Wewe ndiwe ngome yangu.

5Mikononi mwako naiweka roho yangu; Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.

6Nawachukia wao washikao yasiyofaa yenye uongo; Bali mimi namtumaini Bwana.

7Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako, Kwa kuwa umeyaona mateso yangu. Umeijua nafsi yangu taabuni,

8Wala hukunitia mikononi mwa adui; Miguu yangu umeisimamisha panapo nafasi.

9Ee Bwana, unifadhili, maana ni katika dhiki, Jicho langu limenyauka kwa masumbufu, Naam, mwili wangu na nafsi yangu.

10Maana maisha yangu yamekoma kwa huzuni, Na miaka yangu kwa kuugua. Nguvu zangu zinatetemeka kwa uovu wangu, Na mifupa yangu imekauka.

11Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu, Naam, hasa kwa jirani zangu; Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu; Walioniona njiani walinikimbia.

12Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa; Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.

13Maana nimesikia masingizio ya wengi; Hofu ziko pande zote. Waliposhauriana juu yangu, Walifanya hila wauondoe uhai wangu.

14Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.

15Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia.

16Umwangaze mtumishi wako Kwa nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.

17Ee Bwana, nisiaibishwe, maana nimekuita; Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni.

18Midomo ya uongo iwe na ububu, Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi, Kwa majivuno na dharau.

19Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako Ulizowawekea wakuchao; Ulizowatendea wakukimbiliao Mbele ya wanadamu!

20Utawasitiri na fitina za watu Katika sitara ya kuwapo kwako; Utawaficha katika hema Na mashindano ya ndimi.

21Bwana ahimidiwe; kwa maana amenitendea Fadhili za ajabu katika mji wenye boma.

22Nami nalisema kwa haraka yangu, Nimekatiliwa mbali na macho yako; Lakini ulisikia sauti ya dua yangu Wakati nilipokulilia.

23Mpendeni Bwana, Ninyi nyote mlio watauwa wake. Bwana huwahifadhi waaminifu, Humlipa atendaye kiburi malipo tele.

24Iweni hodari, mpige moyo konde, Ninyi nyote mnaomngoja Bwana.